“RAI YANGU
JUU YA ELIMU”
RAI
yangu ni kwamba tunaweza kuifanya nchi yetu kuwa taifa kubwa, na kwamba uwezo
wa kufanya hivyo umo ndani yetu. Tukiifanya nchi yetu kuwa taifa dogo ni kwa
sababu tutakuwa tumejiruhusu kufanya upuuzi badala ya kufanya mambo yenye
muruwa.
Wiki
hii naangalia sifa moja kubwa ya taifa kubwa, sifa ambayo kila taifa kubwa
lazima liwe nayo. Sifa hiyo ni mfumo wa elimu unaoandaa watu watakaokabidhiwa
majukumu ya kuiendesha nchi na kuipeleka mbele. Mfumo wa elimu na maudhui yake
ndilo tanuru linalooka taifa lijalo, na jinsi watoto wanavyoelimishwa ndivyo
taifa linavyojengwa.
Katika
jamii zetu za jadi watoto waliwekewa mfumo wa elimu uliolingana na matakwa ya
jamii zetu za wakati huo. Matakwa hayo yalikuwa ni ya msingi kabisa, ambayo
hayakubeba matarajio na mahitaji ya jamii ya kisasa. Jando na unyago ilikuwa ni
shule ya kutosha kwa mahitaji yetu ya wakati ule.
Kijana
wa kiume alifundishwa jinsi ya kufanya kazi ya ujenzi wa kaya yake, uzalishaji
na ulinzi wa familia yake na jumuiya yake. Kijana wa kike alielekezwa jinsi ya
kufanya kazi zake za nyumbani na jinsi ya kumfanya mume wake awe na furaha
katika mapenzi. Na wote wawili walielekezwa jinsi ya kulea kizazi kilichofuata
katika misingi ile ile iliyowalea wao.
Kwa
jinsi hii, kila kizazi kilikirithisha kizazi kilichokirithi ujuzi, stadi na
maadili yaliyotambulika kama vielelezo vya jamii husika. Kwa kuwa jamii zetu
zilikuwa ni za makabila, na kwa kuwa makabila ndiyo yalikuwa mataifa yetu,
elimu iliyotolewa kwa watoto na vijana ilikuwa ni ile ile kwa kabila zima. Tofauti
baina ya mifumo ya elimu ndiyo iliyoeleza tofauti baina ya makabila, kwa maana
haikuwezekana kuwa na mifumo ya elimu iliyotofautiana ndani ya kabila moja.
Kwa
maana hiyo, basi, elimu ilikuwa ni kiungo cha jamii ndani ya jamii iliyopo, na
vile vile kiungo baina ya jamii iliyopo na ile iliyoitangulia au ile inayokuja.
Ni kiungo hiki kilichokuwa ‘horizontal’ na ‘vertical’ kilichoitambulisha jamii
kama taifa na kilichohakikisha uendelevu wa jamii hiyo.
Vijana
wa jamii yoyote waliosafiri kwenda ughaibuni walitambulika kwa elimu
waliyoidhihirisha na iliyowatofautisha na vijana wengine. Elimu kwa maana hii
haikuishia katika stadi za maisha na ujuzi wa kutenda mambo kama kilimo, uhunzi
au uvuvi, bali pia katika tabia, adabu, heshima na haiba ya kijana. Hata safarini,
mwanajamii alijitambulisha kwa haiba ya jamii yake ambayo ilitokana na elimu
aliyoipata tokea utotoni.
Katika
jamii za kisasa, pamoja na kwamba mambo mengi yamebadilika na tamaduni
zimeingiliana na kuvurugana, bado mataifa yanahangaika kujaribu kuhifadhi
angalau ile misingi inayotambulika kama mihimili ya elimu yake, ambayo
inaendana na utamaduni wake. Kila taifa linalostahili kuitwa taifa linajaribu
kuhifadhi zile sifa zinazolitambulisha kama taifa, tofauti na mataifa mengine,
ule utamaduni unaolifanya lijitambue na litambulike kwa wengine kama taifa.
Hii
ni zaidi ya kujifunza hisabati na sayansi, ni mbali zaidi ya kumiliki
teknolojia ya dijitali. Ni pamoja na tabia, mwenendo, adala na haiba. Ni pamoja
na jinsi ya kuingiliana na kuhusiana na watu, namna ya kuamkia na kusalimia,
namna ya kuongea, namna ya kula, namna ya kujenga urafiki na uchumba.
Mshenzi
mwenye shahada ya chuo kikuu hana elimu, bali ni mshenzi aliyesoma. Anao ujuzi
wa mambo fulani, kama vile uwezo wa kuelezea ni malaika wangapi wanaweza
kucheza ‘sindimba’ juu ya kichwa cha sindano, lakini hana elimu inayomuwezesha
kuishi vyema na jirani zake. Kasoma kweli, na ana ujuzi maridhawa, lakini bado
ni mshenzi. Akikualika kwake huendi, na wewe humualiki kwako.
Nieleweke
kwamba nasema kwamba stadi ni sehemu ya elimu, lakini siyo elimu pekee. Inabidi
iambatane na elimu ya uungwana, tabia njema na haiba yenye staha, inayojali
utu, upendo, huruma, mshikamano na stahamili.
Katika
mazingira yetu ya sasa tunajikuta tukiwa na changamoto kubwa katika suala zima
la elimu kwa ujumla wake kwa maana kwamba tumejikwaza katika elimu ya stadi na
pia tumejikwaza katika elimu ya uungwana. Kwa maana hii, tumepotea mara mbili,
katika kujenga uwezo wa stadi na ufundi, na pia katika kujenga maadili ya
kiungwana. Huku hatuko na huku hatuko.
Ni
vigumu kusema kama nchi yetu inao mfumo wa elimu unaoweza kuelezwa kama mfumo
wa taifa moja linalojenga mustakabali wake. Kila mmoja wetu anayeweza
kujtengenezea mazingira ya kumsomesha (siyo kumuelimisha) mwanawe anafanya
hivyo, jinsi anavyojua mwenyewe, na kwa nyenzo anazozijua mwenyewe.
Shule
zinazoibuka kila mara zinakuja na mitaala yake, na mbali na mitihani ya kitaifa
(kwa shule zinazochagua kuifanya) hakuna jambo linazozifanya zifanane, na kila
shule inazalisha sampuli yake ya Watanzania. Ziko shule zinazozalisha
Watanzania wa Kimarekani, ziko zinazozalisha Watanzania wa Kiingereza,
Watanzania wa Kihindi, wa Kiarabu, wa Kifaransa, wa Kituruki, na kadhalika.
Hizo
shule zinazozalisha Watanzania wasio wa Kitanzania ndizo tunazoambiwa kwamba
zinafundisha vizuri masomo ya stadi. Watoto wanafundishwa hisabati na maarifa
kwa viwango vya juu, na wanatafuna ung’eng’e kama wamezaliwa Oxford! Lakini
watoto hao hawajui hata kuamkia wajomba zao, na baadhi ya tabia zao zinatisha.
Mbali
na hawa watoto wanaotokana na familia zenye uwezo wa kuwasomesha katika shule
hizo za Watanzania wasio wa Kitanzania, sasa tunakutana na wale wanaosoma
katika shule za Watanzania wa Kitanzania, ambao nao ni zahma tupu.
Jenerali Ulimwengu,
13/02/2013
Gazeti la Raia Mwema
No comments:
Post a Comment