WANAOTUMIA
RUNINGA KWA MUDA MREFU HUPOTEZA NGUVU ZA KIUME
WANAUME
wanaotumia muda wa saa tatu na zaidi kwa siku kutazama runinga wanapoteza nguvu
za kiume ukilinganisha na wale wanaotazama runinga mara chache.
Utafiti
uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya ya Umma cha Havard (HSPH) kilichopo Boston
nchini Marekani, umebaini kuwa kuporomoka kwa kiwango cha mbegu za kiume
kunahusiana moja kwa moja na kutofanya mazoezi na kutazama runinga kwa muda
mrefu.
Imeelezwa
kuwa wanaume wanaotazama runinga kwa zaidi ya saa 20 kila wiki wanapoteza
asilimia 44 ya mbegu za kiume ukilinganisha na wale wasiotumia muda mrefu
katika runinga.
Vilevile,
wanaume wanaofanya mazoezi kwa zaidi ya saa 15 kwa wiki, wana uwezo wa kuongeza
asilimia 73 ya mbegu zao ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi au wanaofanya
mazoezi chini ya saa tano kwa wiki.
Kiongozi
wa utafiti huo, Dk Audrey Gaskin alisema mtindo wa maisha unachochea zaidi
upungufu wa mbegu za kiume na uzalishwaji wa mbegu za kiume.
Mtafiti
huyo alifanya uchunguzi wa viwango vya mbegu za kiume za wanaume 189 wenye umri
wa kati ya miaka 18 na 22 kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.
Wanaume
hao walihojiwa kuhusu kiwango cha ufanyaji wao wa mazoezi, muda wanaotumia
katika kutazama runinga au filamu katika kipindi cha miezi mitatu.
“Baada
ya utafiti huo, nusu ya wanaume wasiofanya mazoezi na waliotumia muda mrefu
katika runinga walikuwa na kiwango hafifu cha uzalishaji wa mbegu,” alisema Dk
Gaskin. “Masuala mengine ya kiafya yanayoweza kuathiri kiwango cha mbegu za kiume
ni chakula, msongo wa mawazo na uvutaji wa sigara,” alisema.
Daktari
huyo alisema mwanamume anapokaa kwa muda mrefu katika sofa mbegu za kiume
zinapata kiwango kikubwa cha joto ambalo huathiri uzalishwaji wa mbegu. Alisema
wanaume wanaohitaji watoto wanatakiwa kuacha kuvaa nguo za ndani zinazobana ili
kuimarisha kiwango cha mbegu za kiume huku madereva na waendesha baiskeli
wakionywa kuwa katika hatari ya kupungukiwa kutoa mbegu nyingi.
Mhadhiri
Mkuu katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza, Dk Allan Pacey anasema
matokeo ya utafiti wake yatasaidia kuelimisha umma.
Hata
hivyo, Daktari bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa kwenye Kitengo cha Patholojia
katika Hospitali ya Muhimbili, Henry Mwakyoma aliyewahi kufanya utafiti kuhusu
ugumba kwa wanaume, alisema bado utafiti wa Dk Gaskin una maswali mengi.
“Siwezi
kuukubali au kuukataa utafiti wake, inawezekana ni mionzi au joto ndilo
linalosababisha udhaifu wa mbegu hizo, lakini bado utafiti wake una maswali
mengi,” alisema Dk Mwakyoma.
Alisema mazingira ya eneo husika na hali ya hewa na
mlo vinaweza kusababisha mabadiliko ya kiafya, ikiwemo uzalishwaji wa mbegu za
kiume.
Dk Mwakyoma aliwahi kufanya utafiti katika kipindi
cha Oktoba 2009 hadi Septemba 2010 na kubaini kuwa kati ya wanaume 221
waliopimwa, asilimia 17.2 walikuwa hawana mbegu za kiume kabisa na asilimia
30.03 walikuwa na mbegu dhaifu na chache.
Hivyo basi, asilimia 47.05 ya wanaume waliokwenda kupima katika hospitali hiyo, waligundulika kuwa na matatizo ya ugumba.
Hivyo basi, asilimia 47.05 ya wanaume waliokwenda kupima katika hospitali hiyo, waligundulika kuwa na matatizo ya ugumba.
Dk Mwakyoma alisema sababu za ugumba kwa wanaume
huweza kusababishwa na kuambukizwa kwa vijidudu vya bakteria au virusi katika
tezi inayozalisha mbegu za kiume au magonjwa ya zinaa.
“Baadhi wamezaliwa hivyo, miili yao haizalishi
mbegu au walipata maambukizi ya vijidudu wakati wa kuzaliwa,” alidokeza
Mwakyoma.
Alitaja sababu nyingine zinazosababisha ugumba kwa
wanaume ni kuziba kwa mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka katika
korodani hadi katika uume na kwenda kwa mwanamke.
Sababu nyingine ni mionzi, hasa kwa watu wanaofanya
kazi migodini, jeshini kutokana na baadhi ya kemikali zinazopatikana kwenye
shughuli zao na hasa kuathiri watu wenye umri kuanzia miaka 50 hadi 59.
‘Pia, wanaume waliowahi kuugua ugonjwa wa matezi
nao huathirika katika nyumba ya kuzalisha mbegu,” alisema Dk Mwakyoma.
Naye Injinia John Ben Ngatunga wa Tume ya Mionzi
Tanzania, (TAEC) alisema mionzi iliyopo katika runinga nyingi za kisasa
haziwezi kuleta madhara katika mwili wa binadamu. “Pengine utafiti wake unaweza
kuwa na ukweli iwapo kutazama runinga kutamwathiri mtu kisaikolojia.
Runinga nyingi ni zile zenye LCD (Liquid Crystal)
ambazo hazina athari za mionzi,” aliongeza Ngatunga.
Alisema runinga nyingine zinaweza kuwa na mionzi,
lakini ni pale ambapo mtu ataikaribia kwa umbali wa kati ya inchi saba hadi 12.
Mwananchi: Ijumaa Februari 8, 2013
No comments:
Post a Comment