Saturday, February 16, 2013


WALIOOA WALIOWAZIDI KIPATO HAWANA UFANISI

WANAUME waliooa wanawake wenye mishahara mikubwa au vyeo kuwazidi wao, huathirika kisaikolojia wakati wa tendo la ndoa na wengi wao hutoka nje ya ndoa. Utafiti umebaini.
Utafiti huo uliofanywa katika nchi za Denmark na Marekani umebaini kuwa wanaume wanaopata mshahara mdogo, hawashiriki tendo la ndoa kwa ufanisi na wake zao walio na mishahara mikubwa, ukilinganisha na wanaume walio na kipato kikubwa kuwazidi wake zao.
Msaidizi katika utafiti huo Dk Lamar Pierce ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Mipango katika Chuo Kikuu cha Washington alisema kuwa wanaume huwa dhaifu kiutendaji katika tendo la ndoa, inapotokea mwanamke ana cheo au kipato kikubwa kuliko yeye. Hata hivyo, utafiti huo haukuwahusisha wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa.
Mtafiti huyo alisema kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika, ambapo mfumodume umetawala huku mapinduzi ya kijinsia yakianza kushika kasi.
Dk Pierce alifanya utafiti huo kwa kuchunguza taarifa za sampuli zaidi ya 600,000 za wakazi wa Denmark, ambapo wanandoa wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 49 walichunguzwa, kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.
Ilibainika kuwa kwa mabadiliko ya kijamii katika siku za hivi karibuni, wanawake wamekuwa watafutaji wakuu kuliko wanaume, yamevunja tamaduni na wajibu wa mwanamume, hali inayowaathiri kisaiokolojia wanaume.
“Hamu ya tendo la ndoa na ufanisi vinahusiana kwa karibu na kipato, mitandao ya marafiki, cheo na ile hadhi ya mwanamume kuwa kiongozi katika familia,” alisema.
Akizungumzia utafiti huo Dk Kitila Mkumbo, Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa madhara wanayoyapata wanandoa wa aina hiyo yanasababishwa na tamaduni na mfumodume.
Alisema mila na desturi zinawafanya wanaume wasijiamini pale wanapochangia kidogo katika familia.
“Iwapo mwanamume atamchukulia mke wake kama rafiki na siyo msaidizi wa nyumbani, hawezi kuathirika, tatizo kubwa ni kuwa wanahisi kukosa hadhi ya ‘ubaba’,” alisema Mkumbo.
Alisema kwamba wanaume wengi wa aina hiyo hutoka nje ya ndoa zao kuwatafuta wanawake wanyonge zaidi yao, ambapo hupata faraja ya tendo la ndoa.
Aliongeza: “Wanaume wengi, ambao wake zao wana hadhi na kipato kikubwa, mara kwa mara huwa na hasira, ukali bila sababu, mambo ambayo husababisha waikose raha ya tendo la ndoa kwa wake zao.”
Hata hivyo, Dk Mkumbo alisema kuwa baadhi ya wanawake huonyesha dharau kwa waume zao pindi wanapopandishwa vyeo au kuongeza kipato, jambo linalowaathiri wanaume.“Vyeo, fedha nyingi hasa kwa upande wa wanawake, ndicho chanzo cha kuanguka kwa ndoa nyingi, iwapo tu wanandoa hao hawatakuwa makini,” alisema na kuongeza:
“Wanandoa wanapaswa kuongozwa na upendo, badala ya ndoa yao kuongozwa na mali.”
Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano aliyesajiliwa na Global Source Watch, Dismas Lyassa alisema kwamba utafiti huo una ukweli kwa kiasi kikubwa katika dunia ya sasa.
Alisema kutokana na mila nyingi, hata katika vitabu vya dini mwanamke ameumbwa kama msaidizi na siyo mtafutaji, hivyo mabadiliko hayo yanawaathiri wanaume.
“Zipo familia ambapo mwanamke mwenye kipato anataka kufanya mapenzi pale anapotaka yeye tu, mume wake anapohitaji, yeye husingizia kachoka. Hili linasababisha hata familia hizo ziwe na watoto wachache,” alisema.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitengo cha Saikolojia, Chris Mauki alisema kuwa kipato kinaweza kuathiri ndoa kutokana na tabia za wanandoa.
“Kasumba inaweza kuwa chanzo cha madhara katika ndoa, ambayo mwanamke ana kipato kikubwa. Mwanamume mwenye kipato kidogo anaweza kuhisi tu kuwa, anadunishwa wakati siyo kweli,” alisema Mauki. Alisema kwamba kasumba hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ufanisi katika tendo la ndoa kwa sababu kwa kawaida ugomvi na malumbano, uhusika moja kwa moja na tendo la ndoa.
Watafiti hao walisema kuwa hawana uhakika hasa chanzo cha tatizo hilo, lakini kukosa fahari ya uanaume na mfumodume, huweza kuchochea hasira na kutokujiamini.
Ilibainika kuwa wanaume wengi walitumia viagra au dawa nyingine kuongeza nguvu za kiume, ili waongeze ufanisi kwenye ndoa katika mazingira ambapo, mwanamke ana kipato kikubwa.
Cha ajabu katika utafiti huo ni kuwa, hali hiyo haikuonekana kwa wanandoa ambao mwanamke alikuwa na kipato kikubwa tangu kuanza kwa uhusiano.
Badala yake hali hiyo ilionekana kwa wanandoa ambao awali mwanamke alikuwa na kipato kidogo kisha kikaongezeka wakati wa uhusiano.
Watafiti hao walisema kuwa inawezekana wanaume huathirika kisaikolojia na hutaka kuongeza nguvu ili waonyeshe ufahari wao, ambao wameshindwa kuuonyesha katika kipato.
Alisema mabadiliko hayo huwafanya wanaume kuhisi vyeo vyao vimechukuliwa na hivyo kuathirika kisaikolojia.
Utafiti huo ulifanyika Denmark nchi ambayo inachochea zaidi haki za wanawake.
Hata hivyo, Dk Pierce alisema siyo vyema kuhitimisha kuwa mishahara ya wanawake inawaathiri wanaume wote katika tendo la ndoa, bali wapo wanaopenda kuoa wanawake wenye kipato kikubwa kuwazidi. Mtafiti wa nchini Marekani, Dk Karen Robinson alisema wanawake wenye vipato vikubwa au vyeo katika jamii, wanatakiwa waheshimu hisia za wenza wao, badala ya kuchanganya nafasi zao, kipato katika maisha ya ndoa. “Wanatakiwa waepuke maneno yanayoweza kuudhi au kuchochea mfadhaiko wa kisaikolojia, ili kulinda ndoa,” alisema Dk Robinson.

Mwananchi; Februari 16,  2013

No comments: