Tuesday, February 19, 2013


  Matokeo kidato cha IV vilio kila kona

na Sitta Tumma, Mwanza

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa muda wa siku 14 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.
Kauli hiyo ya CHADEMA imetolewa na mwenyekiti wake taifa, Freeman Mbowe, wakati alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika jana katika viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi.
Mbowe ambaye aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani hapo, alisema, Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kuingia kidato cha kwanza.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Mbowe alisema hili ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.
“Kwa vile Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu na kwa vile watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.
“Kila mwaka wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao. Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.
Alisema, kwa sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao wanakosa fursa ya kuendelea na masomo yao na alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza maendeleo ya nchi na raia wake na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga makubwa mawili ya elimu duni na udini.
Kuhusu Bunge kutoonyeshwa ‘live’, Mbowe alimuonya Spika Anna Makinda na wasaidizi wake kuacha kutumia madaraka yao kuwanyima uhuru na haki wananchi na kwamba Watanzania wanahitaji kuwaona wabunge wao wabovu na wazuri ili mwaka 2015 wafanye maamuzi magumu ya kutokuwachagua au kuwachagua tena.
“Makinda tumemwambia aache ubabaishaji katika uendeshaji wa Bunge. Watanzania wanataka kuwaona wabunge wao wanaolala na wanaoshangilia hoja za hovyo! Tunataka Bunge liendeshwe kwa mazingira yanayomwezesha mwananchi kufahamu kila kitu kinachojadiliwa katika chombo hicho.
Akizungumzia maamuzi ya CHADEMA kuanzisha uongozi wa kikanda, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Hai, alisema sera ya majimbo ni nguzo kubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi, hivyo chama chake hakijakosea kufanya hivyo na wanahitaji Tanzania igawanywe katika uongozi kwa ngazi ya majimbo ili kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Alisema licha ya kwamba sera yao hiyo inabezwa na CCM, lakini ndiyo mkombozi mkubwa katika adha ya umaskini miongoni mwa wananchi, hivyo wataisimamia kikamilifu kuanzia sasa na baada ya kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Mbowe aliishutumu CCM na viongozi wake kwa kueneza siasa mbaya za udini, kwani walianza kuishambulia CUF kwa madai kwamba ni chama cha Kiislamu na baadaye CHADEMA kwamba ni chama cha Wakristo, jambo ambalo kwa sasa limejaa mbegu mbaya ya kuwepo kwa mzozo wa kidini na aliwataka Watanzania kutokubali kugawanywa kwa ukabila, udini na ukanda na wasiichague CCM 2015.
Mbali ya kauli ya Mbowe, matokeo hayo ya kidato cha nne yamelalamikiwa kila kona nchini.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutangaza tatizo la elimu kuwa janga la kitaifa na kumtimua Waziri Kawambwa.
Mbali na Mbatia wadau mbalimbali na wananchi nao wametaka Rais Kikwete kuivunja Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuisuka upya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbatia alisema kuanguka kwa elimu kumetokana na CCM kuendekeza mambo ya ushabiki wa kisiasa hata kwenye mambo yanayolihusu taifa.
Mbatia alieleza kuwa mitaala ndio dira ya elimu lakini akashangazwa na serikali kutokuwa na mitaala rasmi na hata alipolieleza Bunge jambo hilo, wabunge wa CCM walimjia juu na kuamua kuizima hoja hiyo.
“Serikali haijawahi kuwa na mitaala rasmi, taifa halina dira ya elimu; kuna mkanganyiko katika vitabu na ufisadi uliopo unaliangusha taifa hakuna mfumo bali waziri anafanya anavyoamua,” alisema.
Alirejea hoja yake kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kimejiaibisha kukataa hoja yake na kueleza kuwa watoto wengi waliofeli ni wa CCM.
“CCM ndiyo ina majimbo mengi kwa hiyo waliofeli ni watoto wao; sasa badala ya kuhakikisha inaondoa kirusi katika elimu yenyewe inaingiza itikadi za vyama katika suala la elimu.”
Aidha alitaka vitabu vinavyotumika sasa mashuleni, vizuiwe na bajeti ijayo vipengere kumi muhimu iwe ni elimu ili kunusuru anguko la sekta hiyo kwani wizara iliyopo haiwezi kuyatatua peke yake.
Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, kuwa matokeo hayo yameisikitisha serikali haitakuwa na maana yoyote kama haitakuwa na jitihada za makusudi kuikwamua elimu ya Tanzania kutoka katika mfumo uliopo sasa, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafaunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo, alisema serikali imekuwa ikidharau kutatua matatizo ya msingi inayoikabili sekta ya elimu.
Alitaja moja ya matatizo ya walimu ni mazingira mabovu ya kufundishia, hali inayowafanya wengi wao wasiwe na ari ya kufanya kazi hiyo.
“Serikali imeisusa sekta ya elimu na hii ni kwa sababu viongozi wa serikali hawawasomeshi watoto wao katika shule za serikali hivyo hawana uchungu na matatizo yanayowakabili walimu na wanafunzi wa shule hizo,” alisema Lyimo.
Aliongeza kuwa hata katika masuala ya ukaguzi wa maendeleo ya elimu kama ilivyokuwa zamani kwa sasa hautiliwi mkazo kutokana na bajeti finyu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillipo Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo.
Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.
Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.
“Najua kuwa haina uhusiano wa moja kwa moja maana matatizo ya elimu ni makubwa sana nchini. Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko. Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na uharaka katika utendaji kazi, alisema na kuongeza: “…namna hii (zaidi ya nusu ya wahitimu kupata sifuri) na takriban asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja la nne na daraja la sifuri ni mwaka wa tatu sasa mfululizo. Matokeo yakitoka tunasema weeee mpaka povu linatoka.
“Baada ya wiki tumeshasahau na hakuna hatua yoyote. Lazima uwajibikaji utokee,” alisema Zitto.
Alisema ni muhimu Rais Kikwete aichukue Wizara ya Elimu, yaani Waziri wa Elimu awe yeye, pia kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu.
Zitto alisema kuwa Rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.
“Najua wa mwakani ndio wako kidato cha nne sasa na wana msingi mbaya tayari lakini sio jukumu letu kujipa majibu bali ni jukumu letu kuiambia serikali; hapana! Tuwape masharti. Vinginevyo haya yatakwisha na mwakani itakuja,” alisema.
Zitto alisema elimu iliyopo sasa inazalisha matabaka ndani ya jamii na ni hatari kwa uhai wa taifa.
Mbali ya maoni hayo, wadau wengine walimtaka waziri mwenye dhamana ajiuzulu.
Mmoja wa wadau hao Selemani Juma, alisema kadri siku zinavyokwenda ndivyo anguko la elimu linavyozidi kuwa kubwa.
Alisema mvurugano uliopo katika matumizi ya vitabu na kuacha vitabu vilivyokuwa vinatumika na kuanza kutumia vitabu vingine ambavyo alidai vipo kwa ajili ya maslahi ya viongozi, havina ubora na viwango vya kufundishia.
Naye Janeth Alphonce, alieleza kuwa wizara husika chini ya Dk. Kawambwa, haiwezi kutatua mifumo ya elimu ambayo ni ya miaka mingi na haiendani na soko la elimu ya sasa.
Mwalimu John Bosco Katatumba alisema matokeo hayo ni tafsiri ya hali ya ubovu wa elimu nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Akitoa maoni kwa njia ya simu, Lucas Nyangaramila (61), mkazi wa Arusha alisema chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya ni mitaala ya elimu mibovu kwani kila baada ya muda imekuwa ikibadilishwa.
“Mwanafunzi aliyesoma kwa lugha ya Kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kusoma Kiingereza awapo sekondari ni vugumu kwake kuelewa lugha ya Kiingereza mapema na badala yake kuongozwa na wale waliosoma shule za Kiingereza kuanzia shule za msingi,” alisema.
Naye Thobiace Boniface mkazi wa Mbezi Beach jijijini Dar es Salaam, alisema matokeo ni mabaya na yanatia aibu na aliiomba serikali ifute shule za kata kwa sababu ya maandalizi duni.
Hali kadhalika, Mama Saidi mkazi wa Mabibo alisema kukua kwa sayansi na teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa elimu ya wanafunzi kushuka hapa nchini.
“Hii mitandao kama vile intaneti, facebook, twitter n.k bila kusahau simu za mikononi imekuwa ni kikwazo cha elimu kwa watoto wetu kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwasiliana na watu mbalimbali kwenye mitando hiyo, sasa muda wa kujisomea utatoka wapi?” alihoji.
Kwa upande wake David Mlay, alisema kitendo cha shule za serikali kutofanya vizuri hata kwa shule zake za vipaji maalumu ambazo ndizo zilikuwa tegemeo, ni anguko kubwa la elimu nchini.


Chanzo: Tanzania Daima: jumatano, 20 februari 2013

No comments: