TULAANI UBAKAJI, ULAWITI, UPORAJI WANAFUNZI VYUO VIKUU
|
WIKI mbili zilizopita kumekuwa na taarifa za aibu
na za kusikitisha kutokana na mfululizo wa matukio ya ubakaji, ulawiti na
uporaji wa vifaa vya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali hapa
nchini unaoendelea.
Licha ya kwamba ubakaji umekithiri kwa kiasi
kikubwa hapa nchini na hauripotiwi ipasavyo kwenye vyombo vya habari au jamii
hairipoti, lakini haya yanatutia doa.
Kuna matukio kama haya yanawatokea wanajamii huko
vijijini, au makundi yaliyoko pembezoni na hawawezi kupaza sauti au
kuandamana kama wanavyofanya wanafunzi wa vyuo vikuu. Maandamano haya ni
alama ya jinsi ambavyo hali ni mbaya huko vijijini na wananchi walio wengi
wameshateswa na kuumizwa.
Pamoja na matukio haya ya udhalilishaji wa
kijinsia, ya kubakwa kwa wasichana na kulawitiwa kwa wavulana, kumeendelea
kuwepo kwa matukio ya mauaji ya kinyama kama hili la mwanafunzi wa Chuo Kikuu
cha St. John’s cha Dodoma, lililotokea Januari 20, mwaka huu kwa kubakwa na
kuuawa.
Tunajiuliza haki ya raia kuishi iko wapi? Kwanini
waliofanya unyama huu hadi sasa hawajakamatwa na kuchukuliwa hatua? Je,
sheria ya adhabu ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 imefia wapi?
Je, masikini au mwananchi wa kawaida akiuawa hana thamani?
Tukio hili limetanguliwa na matukio kadhaa
yaliyoripotiwa mwaka jana na kusababisha wanafunzi wa chuo hicho kuandamana
hadi Kituo cha Polisi, Mei 30 mwaka jana, ambayo ni ubakaji, ulawiti na
uporaji wa vifaa kama simu, laptop, Tv na redio.
Tunasikitika kuwa hadi leo Jeshi la Polisi
halijachukua hatua za kudhibiti matukio hayo.
Mwaka 2007 nikiwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine
Mwanza, tuliokuwa tukiishi Malimbe, Nganza, Swea, Mkolani na Nyegezi Corner
matukio kama haya yalikuwepo na tuliandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wakati huo
Dk. Alex Msekela, lakini madai yetu hakuyafanyia kazi.Tukio hili limeendelea
hadi Dar es Salaam, na kusababisha wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM) wanaoishi Kigamboni wilayani Temeke, kuandamana kudai ulinzi baada ya
wenzao kubakwa, kulawitiwa na kuporwa vifaa na mali.
Mwaka jana matukio kama haya yameripotiwa katika
vyuo vikuu vya Mt. Augustine (SAUT) Mwanza, RUCO Iringa, na St John’s Dodoma,
lakini hakuna hatua za haraka za kukomesha matukio haya zimechukuliwa.
Wanafunzi wanaoishi nje ya mabweni (Hosteli) ya vyuo vikuu wamekuwa
waathirika wa tatizo la wizi au uporaji.
Matukio ya ubakaji na ulawiti na udhalilishaji wa
kijinsia yameendelea kwa muda mrefu.
Utafiti wa TAMWA uliofanyika mwaka jana katika
visiwa vya Pemba na Unguja umebaini kuwa mwaka 2012 pekee kulikuwa na matukio
400 ya ubakaji, wakati Mkoa wa Kilimanjaro pekee ulikuwa na kesi 46 za ubakaji
zilizoripotiwa polisi.
Lakini hatuchunguzi kwa kina wanawake, wasichana,
vikongwe, na watoto masikini walioko vijijini ambao wanabakwa usiku na mchana
na habari zao hazitangazwi.
Jamii nzima tuungane kulaani matukio haya
yanayoendelea, tuwalaani viongozi waliotakiwa kuchukua hatua za kulimaliza
tatizo hili na hawafanyi hivyo.
Jamii ikatae unyanyasaji, na kukumbatiwa kwa
wahuni au wahalifu wa aina hii ambao wanatuharibia taifa letu.
Tunajua kuwa kitendo cha udhalilishaji kijinsia
kinaathiri kisaikolojia na kama wasomi wanabakwa, tunadidimiza nguvu kazi ya
taifa hili.
Je, kama tunakuwa na wasomi waliochanganyikiwa
kwa kuumizwa kisaikolojia tunaandaa taifa gani? Si kwamba ni mwanzo wa kuwa
masikini zaidi?
Kutokana na matukio haya ya aibu ambayo
yanalidhalilisha taifa letu, sisi kama wanajamii tunapaswa kulaani na
kulitaka Jeshi la Polisi kuwawajibisha viongozi na wakuu wa vituo ambao
wamepokea malalamiko ya wanafunzi wa vyuo vikuu, Kigambani na Dodoma na
hawakuchukua hatua.
Pia Jeshi la Polisi liache kupuuza madai ya
wananchi juu ya wizi unaotokea na kufanya kazi yake ya kulinda raia na mali
zao.
Jeshi la Polisi liache kutumia nguvu kubwa
kuwasambaratisha wananchi wanaodai haki badala yake nguvu zitumike kuwalinda
kama ilivyofanyika Kigamboni juzi.
Inashangaza kuona wanafunzi wanadai ulinzi wa
askari watatu wananyimwa, lakini wakiandamana, askari 500 wanapelekwa
kuwapiga mabomu.
Uongozi wa serikali za mitaa na vijiji ambao
matukio hayo yanafanyika, wawajibike kwa kushindwa kusimamia kikamilifu
ulinzi wa raia na mali zao, na serikali kuu ihakikishe inaboresha mazingira
ya ulinzi, upatikanaji wa vituo vya polisi na vitendea kazi katika mazingira
hatarishi hasa wanakoishi wanafunzi.
Tuchukue hatua haraka inavyowezekana kudhibiti
matukio haya, na sote tuseme ‘hapana ubakaji kwa Watanzania wote!’
|
Deogratius Temba Mwananchi: jumapili, 27 januari 2013
No comments:
Post a Comment