Wednesday, February 27, 2013


ALBINO AUAWA, WAWILI WAKATWA VIUNGO

Vicky Ntetema

HALI ya wasiwasi imetanda miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, baada ya watu watatu kukatwa viungo na mmoja wao kuuawa mwezi huu.


Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya albino 72 wameuawa, 34 wamenusurika, wengi wao kwa kukatwa viungo au kuumizwa. Makaburi 15 yamefukuliwa na viungo kuchukuliwa na kumekuwa na majaribio manne ya kufukua makaburi.
Katika matukio ya hivi karibuni, walemavu hao wakazi wa Tabora na Sumbawanga wamekatwa mikono ya kushoto. Ukatili huo safari hii umekwenda kinyume na ilivyokuwa mwaka 2010-2011 wakati mikono ya kuume ndiyo iliyokuwa inakisiwa.
Aliyeuawa ni
Lugolola Bunzari (7) na waliojeruhiwa ni Mwigulu Matonange (10) na Maria Chambanenge (39).

Katika matukio hayo, mtoto mwenye umri wa miezi saba alinusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya mama yake usiku katika eneo la Lamadi, Wilaya ya Busega, Mwanza siku moja baada ya kupokea ujumbe mfupi wa simu kwamba mtoto wake anawindwa.

Marehemu Lugolola
Kijiji cha Kanoge kina umbali wa takriban kilomita 75 kutoka Tabora Mjini, barabara iendayo Ulyankulu kwenye machimbo ya dhahabu.
Imenichukua saa mbili na nusu kufika huko. Saa moja na nusu kati ya hizo, nilizitumia katika safari ya kilomita 15 tu kutoka Kanoge makao makuu ya kijiji hadi Kitongoji cha Kinondoni alikouawa mtoto Lugolola.

Nyumbani kwa Bunzari niliwakuta ndugu na jamaa kutoka vijiji vya jirani vya Wilaya hiyo ya Kaliua, Tabora. Bibi mzaa baba wa Lugolola, Gama Zengabuyanda (60), ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka Hospitali ya Mkoa ya Kitete alikokuwa akitibiwa baada ya kushambuliwa na majambazi alipotaka kumwokoa mjukuu wake.

Huku akilia kwa huzuni, Zengabuyanda alinisimulia jinsi mjukuu wake na baba yake mzazi, Zengabuyanda Meli (95) walivyouawa kikatili.

Katika muda wa kati ya saa 10 na 11 alfajiri ya kuamkia Februari Mosi mwaka huu, Lugolola aliuawa kikatili baada ya kukatwa mkono kwa panga, kukwanguliwa nywele, kujeruhiwa mkono wa kulia na sikioni na kuondolewa ngozi kwenye sehemu ya paji la uso.

Katika mashambulizi hayo, babu yake Meli pia aliuawa alipojaribu kumwokoa mjukuu wake. Vilevile baba yake mzazi, Bunzari Shinga alijeruhiwa wakati alipojaribu kumlinda mwanaye.
Nilimkuta mama mzazi wa Lugolola aitwaye Kulwa akisaidiana na ndugu zake kumenya maharage mabichi waliyoyatoa shambani mwao muda mfupi tu uliopita.

Yeye ni mke mkubwa wa Bunzari Shinga (35). Walibahatika kupata watoto sita, wawili kati yao ni albino. Lugolola na marehemu mdogo wake aitwaye Maganga aliyefariki kwa malaria mwaka 2011.

Usiku wa mashambulizi hayo, Kulwa anasema alikuwa amelala na watoto wake wadogo wa kike (mmoja, Shija mkubwa) na Lugolola kwenye nyumba yake inayotazamana na ile ya mke mwenzake Pili, umbali wa takriban mita 20. Bunzari alikuwa amelala kwa mke huyo mdogo na binti yao mwenye umri wa mwaka mmoja hivi.

Mzee Meli alikuwa amelala na watoto wa kiume upande wa kulia wa nyumba ya Kulwa.
“Aliamshwa usingizini na kelele za watoto waliokuwa wakilalamika kwamba wanapigwa na fimbo. Alipotaka kwenda chumbani kwa watoto alishambuliwa kwa mapanga kichwani, usoni, mgongoni, mikononi na miguuni,” Gama anaelezea huku akilia.
“Pamoja na hayo yote, Baba alijikongoja kuelekea kwenye nyumba alimolala mjukuu wangu, Lugolola huku akipiga mayowe, Tumevamiwa! Nani anataka kuwadhuru watoto wangu.”
Majangili hayo yakamshambulia zaidi kwa mapanga na marungu na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Jamani Baba yangu!”
Gama anasema alikuwa amelala kwenye banda lake lililopo kati ya nyumba ya pili na ile ya babu.

Banda hilo la nyasi na kuta za udongo na miti lilikuwa limepambwa kwa vibuyu vya aina mbalimbali, tunguri, vyungu vilivyohifadhi mizizi, magamba ya miti, kauri (nyumba za konokono), hirizi, nywele za binadamu, taya za wanyama, vipande vya mifupa mbalimbali, fuvu la mnyama na gamba la kobe. Katika mazungumzo yetu niligundua kwamba Mzee Meli alikuwa mganga wa kienyeji.

Gama aliposikia vilio vya watoto alitoka nyumbani mwake na kukimbilia kwenye nyumba ya babu ili kujua kilichowatokea wajukuu wake na sababu iliyomfanya baba yake apige mayowe.

Akiwa nje alimwona baba yake akishambuliwa na watu watatu. Watu wengine wanne walikuwa wamesimama nje ya nyumba ya Kulwa wakiwa wameshika silaha mbalimbali ikiwa ni pamoja na magobole, mapanga na marungu. Gama alipiga kelele, ‘Tumevamiwa!’ na mmoja kati ya watu hao alimshambulia kwa panga kichwani, miguuni na mikononi.
Alianguka na akapata mwanya wa kutambaa chini kwa chini kama nyoka hadi akafika kwenye shamba la mahindi na kupotelea kwenye vichaka.
Hata hivyo, alizimia na alipozinduka alijikuta akiwa Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Kitete.

Gama alikuwa amefiwa na mjukuu wake na baba yake mzazi. Kinachomsikitisha zaidi ni kwamba waliuawa bila ya hatia na hakupata hata fursa ya kuwaaga na kuwazika.
Itaendelea kesho...

Mwananchi: Jumatano Februari 27,  2013

Tuesday, February 19, 2013


  Matokeo kidato cha IV vilio kila kona

na Sitta Tumma, Mwanza

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa muda wa siku 14 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.
Kauli hiyo ya CHADEMA imetolewa na mwenyekiti wake taifa, Freeman Mbowe, wakati alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika jana katika viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi.
Mbowe ambaye aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani hapo, alisema, Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kuingia kidato cha kwanza.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Mbowe alisema hili ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.
“Kwa vile Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu na kwa vile watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.
“Kila mwaka wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao. Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.
Alisema, kwa sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao wanakosa fursa ya kuendelea na masomo yao na alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza maendeleo ya nchi na raia wake na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga makubwa mawili ya elimu duni na udini.
Kuhusu Bunge kutoonyeshwa ‘live’, Mbowe alimuonya Spika Anna Makinda na wasaidizi wake kuacha kutumia madaraka yao kuwanyima uhuru na haki wananchi na kwamba Watanzania wanahitaji kuwaona wabunge wao wabovu na wazuri ili mwaka 2015 wafanye maamuzi magumu ya kutokuwachagua au kuwachagua tena.
“Makinda tumemwambia aache ubabaishaji katika uendeshaji wa Bunge. Watanzania wanataka kuwaona wabunge wao wanaolala na wanaoshangilia hoja za hovyo! Tunataka Bunge liendeshwe kwa mazingira yanayomwezesha mwananchi kufahamu kila kitu kinachojadiliwa katika chombo hicho.
Akizungumzia maamuzi ya CHADEMA kuanzisha uongozi wa kikanda, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Hai, alisema sera ya majimbo ni nguzo kubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi, hivyo chama chake hakijakosea kufanya hivyo na wanahitaji Tanzania igawanywe katika uongozi kwa ngazi ya majimbo ili kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Alisema licha ya kwamba sera yao hiyo inabezwa na CCM, lakini ndiyo mkombozi mkubwa katika adha ya umaskini miongoni mwa wananchi, hivyo wataisimamia kikamilifu kuanzia sasa na baada ya kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Mbowe aliishutumu CCM na viongozi wake kwa kueneza siasa mbaya za udini, kwani walianza kuishambulia CUF kwa madai kwamba ni chama cha Kiislamu na baadaye CHADEMA kwamba ni chama cha Wakristo, jambo ambalo kwa sasa limejaa mbegu mbaya ya kuwepo kwa mzozo wa kidini na aliwataka Watanzania kutokubali kugawanywa kwa ukabila, udini na ukanda na wasiichague CCM 2015.
Mbali ya kauli ya Mbowe, matokeo hayo ya kidato cha nne yamelalamikiwa kila kona nchini.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutangaza tatizo la elimu kuwa janga la kitaifa na kumtimua Waziri Kawambwa.
Mbali na Mbatia wadau mbalimbali na wananchi nao wametaka Rais Kikwete kuivunja Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuisuka upya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbatia alisema kuanguka kwa elimu kumetokana na CCM kuendekeza mambo ya ushabiki wa kisiasa hata kwenye mambo yanayolihusu taifa.
Mbatia alieleza kuwa mitaala ndio dira ya elimu lakini akashangazwa na serikali kutokuwa na mitaala rasmi na hata alipolieleza Bunge jambo hilo, wabunge wa CCM walimjia juu na kuamua kuizima hoja hiyo.
“Serikali haijawahi kuwa na mitaala rasmi, taifa halina dira ya elimu; kuna mkanganyiko katika vitabu na ufisadi uliopo unaliangusha taifa hakuna mfumo bali waziri anafanya anavyoamua,” alisema.
Alirejea hoja yake kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kimejiaibisha kukataa hoja yake na kueleza kuwa watoto wengi waliofeli ni wa CCM.
“CCM ndiyo ina majimbo mengi kwa hiyo waliofeli ni watoto wao; sasa badala ya kuhakikisha inaondoa kirusi katika elimu yenyewe inaingiza itikadi za vyama katika suala la elimu.”
Aidha alitaka vitabu vinavyotumika sasa mashuleni, vizuiwe na bajeti ijayo vipengere kumi muhimu iwe ni elimu ili kunusuru anguko la sekta hiyo kwani wizara iliyopo haiwezi kuyatatua peke yake.
Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, kuwa matokeo hayo yameisikitisha serikali haitakuwa na maana yoyote kama haitakuwa na jitihada za makusudi kuikwamua elimu ya Tanzania kutoka katika mfumo uliopo sasa, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafaunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo, alisema serikali imekuwa ikidharau kutatua matatizo ya msingi inayoikabili sekta ya elimu.
Alitaja moja ya matatizo ya walimu ni mazingira mabovu ya kufundishia, hali inayowafanya wengi wao wasiwe na ari ya kufanya kazi hiyo.
“Serikali imeisusa sekta ya elimu na hii ni kwa sababu viongozi wa serikali hawawasomeshi watoto wao katika shule za serikali hivyo hawana uchungu na matatizo yanayowakabili walimu na wanafunzi wa shule hizo,” alisema Lyimo.
Aliongeza kuwa hata katika masuala ya ukaguzi wa maendeleo ya elimu kama ilivyokuwa zamani kwa sasa hautiliwi mkazo kutokana na bajeti finyu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillipo Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo.
Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.
Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.
“Najua kuwa haina uhusiano wa moja kwa moja maana matatizo ya elimu ni makubwa sana nchini. Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko. Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na uharaka katika utendaji kazi, alisema na kuongeza: “…namna hii (zaidi ya nusu ya wahitimu kupata sifuri) na takriban asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja la nne na daraja la sifuri ni mwaka wa tatu sasa mfululizo. Matokeo yakitoka tunasema weeee mpaka povu linatoka.
“Baada ya wiki tumeshasahau na hakuna hatua yoyote. Lazima uwajibikaji utokee,” alisema Zitto.
Alisema ni muhimu Rais Kikwete aichukue Wizara ya Elimu, yaani Waziri wa Elimu awe yeye, pia kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu.
Zitto alisema kuwa Rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.
“Najua wa mwakani ndio wako kidato cha nne sasa na wana msingi mbaya tayari lakini sio jukumu letu kujipa majibu bali ni jukumu letu kuiambia serikali; hapana! Tuwape masharti. Vinginevyo haya yatakwisha na mwakani itakuja,” alisema.
Zitto alisema elimu iliyopo sasa inazalisha matabaka ndani ya jamii na ni hatari kwa uhai wa taifa.
Mbali ya maoni hayo, wadau wengine walimtaka waziri mwenye dhamana ajiuzulu.
Mmoja wa wadau hao Selemani Juma, alisema kadri siku zinavyokwenda ndivyo anguko la elimu linavyozidi kuwa kubwa.
Alisema mvurugano uliopo katika matumizi ya vitabu na kuacha vitabu vilivyokuwa vinatumika na kuanza kutumia vitabu vingine ambavyo alidai vipo kwa ajili ya maslahi ya viongozi, havina ubora na viwango vya kufundishia.
Naye Janeth Alphonce, alieleza kuwa wizara husika chini ya Dk. Kawambwa, haiwezi kutatua mifumo ya elimu ambayo ni ya miaka mingi na haiendani na soko la elimu ya sasa.
Mwalimu John Bosco Katatumba alisema matokeo hayo ni tafsiri ya hali ya ubovu wa elimu nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Akitoa maoni kwa njia ya simu, Lucas Nyangaramila (61), mkazi wa Arusha alisema chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya ni mitaala ya elimu mibovu kwani kila baada ya muda imekuwa ikibadilishwa.
“Mwanafunzi aliyesoma kwa lugha ya Kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kusoma Kiingereza awapo sekondari ni vugumu kwake kuelewa lugha ya Kiingereza mapema na badala yake kuongozwa na wale waliosoma shule za Kiingereza kuanzia shule za msingi,” alisema.
Naye Thobiace Boniface mkazi wa Mbezi Beach jijijini Dar es Salaam, alisema matokeo ni mabaya na yanatia aibu na aliiomba serikali ifute shule za kata kwa sababu ya maandalizi duni.
Hali kadhalika, Mama Saidi mkazi wa Mabibo alisema kukua kwa sayansi na teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa elimu ya wanafunzi kushuka hapa nchini.
“Hii mitandao kama vile intaneti, facebook, twitter n.k bila kusahau simu za mikononi imekuwa ni kikwazo cha elimu kwa watoto wetu kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwasiliana na watu mbalimbali kwenye mitando hiyo, sasa muda wa kujisomea utatoka wapi?” alihoji.
Kwa upande wake David Mlay, alisema kitendo cha shule za serikali kutofanya vizuri hata kwa shule zake za vipaji maalumu ambazo ndizo zilikuwa tegemeo, ni anguko kubwa la elimu nchini.


Chanzo: Tanzania Daima: jumatano, 20 februari 2013

Monday, February 18, 2013

RAI YANGU JUU YA ELIMU


“RAI YANGU JUU YA ELIMU”

RAI yangu ni kwamba tunaweza kuifanya nchi yetu kuwa taifa kubwa, na kwamba uwezo wa kufanya hivyo umo ndani yetu. Tukiifanya nchi yetu kuwa taifa dogo ni kwa sababu tutakuwa tumejiruhusu kufanya upuuzi badala ya kufanya mambo yenye muruwa.
Wiki hii naangalia sifa moja kubwa ya taifa kubwa, sifa ambayo kila taifa kubwa lazima liwe nayo. Sifa hiyo ni mfumo wa elimu unaoandaa watu watakaokabidhiwa majukumu ya kuiendesha nchi na kuipeleka mbele. Mfumo wa elimu na maudhui yake ndilo tanuru linalooka taifa lijalo, na jinsi watoto wanavyoelimishwa ndivyo taifa linavyojengwa.
Katika jamii zetu za jadi watoto waliwekewa mfumo wa elimu uliolingana na matakwa ya jamii zetu za wakati huo. Matakwa hayo yalikuwa ni ya msingi kabisa, ambayo hayakubeba matarajio na mahitaji ya jamii ya kisasa. Jando na unyago ilikuwa ni shule ya kutosha kwa mahitaji yetu ya wakati ule.
Kijana wa kiume alifundishwa jinsi ya kufanya kazi ya ujenzi wa kaya yake, uzalishaji na ulinzi wa familia yake na jumuiya yake. Kijana wa kike alielekezwa jinsi ya kufanya kazi zake za nyumbani na jinsi ya kumfanya mume wake awe na furaha katika mapenzi. Na wote wawili walielekezwa jinsi ya kulea kizazi kilichofuata katika misingi ile ile iliyowalea wao.
Kwa jinsi hii, kila kizazi kilikirithisha kizazi kilichokirithi ujuzi, stadi na maadili yaliyotambulika kama vielelezo vya jamii husika. Kwa kuwa jamii zetu zilikuwa ni za makabila, na kwa kuwa makabila ndiyo yalikuwa mataifa yetu, elimu iliyotolewa kwa watoto na vijana ilikuwa ni ile ile kwa kabila zima. Tofauti baina ya mifumo ya elimu ndiyo iliyoeleza tofauti baina ya makabila, kwa maana haikuwezekana kuwa na mifumo ya elimu iliyotofautiana ndani ya kabila moja.
Kwa maana hiyo, basi, elimu ilikuwa ni kiungo cha jamii ndani ya jamii iliyopo, na vile vile kiungo baina ya jamii iliyopo na ile iliyoitangulia au ile inayokuja. Ni kiungo hiki kilichokuwa ‘horizontal’ na ‘vertical’ kilichoitambulisha jamii kama taifa na kilichohakikisha uendelevu wa jamii hiyo.
Vijana wa jamii yoyote waliosafiri kwenda ughaibuni walitambulika kwa elimu waliyoidhihirisha na iliyowatofautisha na vijana wengine. Elimu kwa maana hii haikuishia katika stadi za maisha na ujuzi wa kutenda mambo kama kilimo, uhunzi au uvuvi, bali pia katika tabia, adabu, heshima na haiba ya kijana. Hata safarini, mwanajamii alijitambulisha kwa haiba ya jamii yake ambayo ilitokana na elimu aliyoipata tokea utotoni.
Katika jamii za kisasa, pamoja na kwamba mambo mengi yamebadilika na tamaduni zimeingiliana na kuvurugana, bado mataifa yanahangaika kujaribu kuhifadhi angalau ile misingi inayotambulika kama mihimili ya elimu yake, ambayo inaendana na utamaduni wake. Kila taifa linalostahili kuitwa taifa linajaribu kuhifadhi zile sifa zinazolitambulisha kama taifa, tofauti na mataifa mengine, ule utamaduni unaolifanya lijitambue na litambulike kwa wengine kama taifa.
Hii ni zaidi ya kujifunza hisabati na sayansi, ni mbali zaidi ya kumiliki teknolojia ya dijitali. Ni pamoja na tabia, mwenendo, adala na haiba. Ni pamoja na jinsi ya kuingiliana na kuhusiana na watu, namna ya kuamkia na kusalimia, namna ya kuongea, namna ya kula, namna ya kujenga urafiki na uchumba.
Mshenzi mwenye shahada ya chuo kikuu hana elimu, bali ni mshenzi aliyesoma. Anao ujuzi wa mambo fulani, kama vile uwezo wa kuelezea ni malaika wangapi wanaweza kucheza ‘sindimba’ juu ya kichwa cha sindano, lakini hana elimu inayomuwezesha kuishi vyema na jirani zake. Kasoma kweli, na ana ujuzi maridhawa, lakini bado ni mshenzi. Akikualika kwake huendi, na wewe humualiki kwako.
Nieleweke kwamba nasema kwamba stadi ni sehemu ya elimu, lakini siyo elimu pekee. Inabidi iambatane na elimu ya uungwana, tabia njema na haiba yenye staha, inayojali utu, upendo, huruma, mshikamano na stahamili.
Katika mazingira yetu ya sasa tunajikuta tukiwa na changamoto kubwa katika suala zima la elimu kwa ujumla wake kwa maana kwamba tumejikwaza katika elimu ya stadi na pia tumejikwaza katika elimu ya uungwana. Kwa maana hii, tumepotea mara mbili, katika kujenga uwezo wa stadi na ufundi, na pia katika kujenga maadili ya kiungwana. Huku hatuko na huku hatuko.
Ni vigumu kusema kama nchi yetu inao mfumo wa elimu unaoweza kuelezwa kama mfumo wa taifa moja linalojenga mustakabali wake. Kila mmoja wetu anayeweza kujtengenezea mazingira ya kumsomesha (siyo kumuelimisha) mwanawe anafanya hivyo, jinsi anavyojua mwenyewe, na kwa nyenzo anazozijua mwenyewe.
Shule zinazoibuka kila mara zinakuja na mitaala yake, na mbali na mitihani ya kitaifa (kwa shule zinazochagua kuifanya) hakuna jambo linazozifanya zifanane, na kila shule inazalisha sampuli yake ya Watanzania. Ziko shule zinazozalisha Watanzania wa Kimarekani, ziko zinazozalisha Watanzania wa Kiingereza, Watanzania wa Kihindi, wa Kiarabu, wa Kifaransa, wa Kituruki, na kadhalika.
Hizo shule zinazozalisha Watanzania wasio wa Kitanzania ndizo tunazoambiwa kwamba zinafundisha vizuri masomo ya stadi. Watoto wanafundishwa hisabati na maarifa kwa viwango vya juu, na wanatafuna ung’eng’e kama wamezaliwa Oxford! Lakini watoto hao hawajui hata kuamkia wajomba zao, na baadhi ya tabia zao zinatisha.
Mbali na hawa watoto wanaotokana na familia zenye uwezo wa kuwasomesha katika shule hizo za Watanzania wasio wa Kitanzania, sasa tunakutana na wale wanaosoma katika shule za Watanzania wa Kitanzania, ambao nao ni zahma tupu.

Jenerali Ulimwengu, 13/02/2013
Gazeti la Raia Mwema

Saturday, February 16, 2013


WALIOOA WALIOWAZIDI KIPATO HAWANA UFANISI

WANAUME waliooa wanawake wenye mishahara mikubwa au vyeo kuwazidi wao, huathirika kisaikolojia wakati wa tendo la ndoa na wengi wao hutoka nje ya ndoa. Utafiti umebaini.
Utafiti huo uliofanywa katika nchi za Denmark na Marekani umebaini kuwa wanaume wanaopata mshahara mdogo, hawashiriki tendo la ndoa kwa ufanisi na wake zao walio na mishahara mikubwa, ukilinganisha na wanaume walio na kipato kikubwa kuwazidi wake zao.
Msaidizi katika utafiti huo Dk Lamar Pierce ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Mipango katika Chuo Kikuu cha Washington alisema kuwa wanaume huwa dhaifu kiutendaji katika tendo la ndoa, inapotokea mwanamke ana cheo au kipato kikubwa kuliko yeye. Hata hivyo, utafiti huo haukuwahusisha wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa.
Mtafiti huyo alisema kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika, ambapo mfumodume umetawala huku mapinduzi ya kijinsia yakianza kushika kasi.
Dk Pierce alifanya utafiti huo kwa kuchunguza taarifa za sampuli zaidi ya 600,000 za wakazi wa Denmark, ambapo wanandoa wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 49 walichunguzwa, kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.
Ilibainika kuwa kwa mabadiliko ya kijamii katika siku za hivi karibuni, wanawake wamekuwa watafutaji wakuu kuliko wanaume, yamevunja tamaduni na wajibu wa mwanamume, hali inayowaathiri kisaiokolojia wanaume.
“Hamu ya tendo la ndoa na ufanisi vinahusiana kwa karibu na kipato, mitandao ya marafiki, cheo na ile hadhi ya mwanamume kuwa kiongozi katika familia,” alisema.
Akizungumzia utafiti huo Dk Kitila Mkumbo, Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa madhara wanayoyapata wanandoa wa aina hiyo yanasababishwa na tamaduni na mfumodume.
Alisema mila na desturi zinawafanya wanaume wasijiamini pale wanapochangia kidogo katika familia.
“Iwapo mwanamume atamchukulia mke wake kama rafiki na siyo msaidizi wa nyumbani, hawezi kuathirika, tatizo kubwa ni kuwa wanahisi kukosa hadhi ya ‘ubaba’,” alisema Mkumbo.
Alisema kwamba wanaume wengi wa aina hiyo hutoka nje ya ndoa zao kuwatafuta wanawake wanyonge zaidi yao, ambapo hupata faraja ya tendo la ndoa.
Aliongeza: “Wanaume wengi, ambao wake zao wana hadhi na kipato kikubwa, mara kwa mara huwa na hasira, ukali bila sababu, mambo ambayo husababisha waikose raha ya tendo la ndoa kwa wake zao.”
Hata hivyo, Dk Mkumbo alisema kuwa baadhi ya wanawake huonyesha dharau kwa waume zao pindi wanapopandishwa vyeo au kuongeza kipato, jambo linalowaathiri wanaume.“Vyeo, fedha nyingi hasa kwa upande wa wanawake, ndicho chanzo cha kuanguka kwa ndoa nyingi, iwapo tu wanandoa hao hawatakuwa makini,” alisema na kuongeza:
“Wanandoa wanapaswa kuongozwa na upendo, badala ya ndoa yao kuongozwa na mali.”
Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano aliyesajiliwa na Global Source Watch, Dismas Lyassa alisema kwamba utafiti huo una ukweli kwa kiasi kikubwa katika dunia ya sasa.
Alisema kutokana na mila nyingi, hata katika vitabu vya dini mwanamke ameumbwa kama msaidizi na siyo mtafutaji, hivyo mabadiliko hayo yanawaathiri wanaume.
“Zipo familia ambapo mwanamke mwenye kipato anataka kufanya mapenzi pale anapotaka yeye tu, mume wake anapohitaji, yeye husingizia kachoka. Hili linasababisha hata familia hizo ziwe na watoto wachache,” alisema.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitengo cha Saikolojia, Chris Mauki alisema kuwa kipato kinaweza kuathiri ndoa kutokana na tabia za wanandoa.
“Kasumba inaweza kuwa chanzo cha madhara katika ndoa, ambayo mwanamke ana kipato kikubwa. Mwanamume mwenye kipato kidogo anaweza kuhisi tu kuwa, anadunishwa wakati siyo kweli,” alisema Mauki. Alisema kwamba kasumba hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ufanisi katika tendo la ndoa kwa sababu kwa kawaida ugomvi na malumbano, uhusika moja kwa moja na tendo la ndoa.
Watafiti hao walisema kuwa hawana uhakika hasa chanzo cha tatizo hilo, lakini kukosa fahari ya uanaume na mfumodume, huweza kuchochea hasira na kutokujiamini.
Ilibainika kuwa wanaume wengi walitumia viagra au dawa nyingine kuongeza nguvu za kiume, ili waongeze ufanisi kwenye ndoa katika mazingira ambapo, mwanamke ana kipato kikubwa.
Cha ajabu katika utafiti huo ni kuwa, hali hiyo haikuonekana kwa wanandoa ambao mwanamke alikuwa na kipato kikubwa tangu kuanza kwa uhusiano.
Badala yake hali hiyo ilionekana kwa wanandoa ambao awali mwanamke alikuwa na kipato kidogo kisha kikaongezeka wakati wa uhusiano.
Watafiti hao walisema kuwa inawezekana wanaume huathirika kisaikolojia na hutaka kuongeza nguvu ili waonyeshe ufahari wao, ambao wameshindwa kuuonyesha katika kipato.
Alisema mabadiliko hayo huwafanya wanaume kuhisi vyeo vyao vimechukuliwa na hivyo kuathirika kisaikolojia.
Utafiti huo ulifanyika Denmark nchi ambayo inachochea zaidi haki za wanawake.
Hata hivyo, Dk Pierce alisema siyo vyema kuhitimisha kuwa mishahara ya wanawake inawaathiri wanaume wote katika tendo la ndoa, bali wapo wanaopenda kuoa wanawake wenye kipato kikubwa kuwazidi. Mtafiti wa nchini Marekani, Dk Karen Robinson alisema wanawake wenye vipato vikubwa au vyeo katika jamii, wanatakiwa waheshimu hisia za wenza wao, badala ya kuchanganya nafasi zao, kipato katika maisha ya ndoa. “Wanatakiwa waepuke maneno yanayoweza kuudhi au kuchochea mfadhaiko wa kisaikolojia, ili kulinda ndoa,” alisema Dk Robinson.

Mwananchi; Februari 16,  2013