‘WAZAZI KIKWAZO
KUPOROMOKA MAADILI YA WATOTO’
na
Danson Kaijage, Dodoma
|
UZEMBE wa wazazi na walezi kushindwa kuwalea
watoto wao katika misingi bora ya kimaadili umeelezwa kusababisha kuporomoka
kwa maadili ya watoto nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya
Bahi, Betty Mkwasa alipokuwa akizungumza na wazazi wa watoto wa shule ya
msingi ya St. Ignatius katika mahafali ya tatu ya darasa la saba katika shule
hiyo.
Alisema kuwa hivi sasa wazazi wamekuwa
wakilalamika kwa madai kuwa watoto wengi wamepoteza maadili ya Mtanzania
lakini wazazi
hao na walezi wamesahau kuwa hawana muda wa kuzungumza nao.
Aliongeza kuwa wazazi wengi wamejijengea tabia ya
kuwapeleka watoto wao katika shule za bweni kuanzia shule ya chekechea jambo
ambalo linawanyima fursa ya kukaa na wazazi wao.
“Mimi nashangaa yaani wazazi wengi wanawapeleka
watoto wao katika shule hizi za bweni mtoto akiwa mdogo kabisa kuanzia
chekechea hadi Chuo Kikuu, sasa kwa hali hiyo unafikiria mtoto ataweza kujua
hata mila za
familia husika kweli.
“Yaani wazazi wamegeuza walimu kama ni wazazi
kamili wa watoto, wazazi wengi hawana muda kabisa wa kukaa na watoto
wao wakawasikiliza
kujua wana mawazo gani, matokeo yake watoto wanakuwa na tabia zao na hawana uelewa
juu ya mila na desturi husika za familia au kabila,” alisema.
Aliwataka wazazi kuwa karibu na walimu ili kuweza kubaini
matatizo ambayo yanaweza kujitokeza pindi watoto wawapo shuleni ikiwemo kujua
maendeleo ya mtoto wake.
|
jumatatu, 20 agosti 2012, Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment