MWANAFUNZI AFIA GESTI AKITOLEWA MIMBA
GAZETI LA MWANANCHI Alhamisi Decemba 27, 2012
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika
shule ya Sekondari ya Tongoni nje kidogo ya jiji la Tanga, (jina
tunalihifadhi) amekutwa amekufa ndani ya nyumba ya kulala wageni alikopelekwa
kutolewa mimba bila mafanikio.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na
kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe
mwanafunzi huyo alikutwa amekufa juzi katika nyumba ya kulala wageni iliyopo
barabara ya 21 jijini Tanga.
Mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema kwamba mwanafunzi huyo aliingia
saa 4.00 asubuhi siku ya tukio akiwa ameambatana na kijana mmoja wakakodi
chumba.
“Baadaye alikuja mwanaume mmoja wa makamo ambaye
alituuliza kama wameingia mwanafunzi huyo na mwenzake, tulipomwonyesha
chumba walichoingia naye akakodi chumba cha jirani ndipo tukaona wote
wakijifungia kwenye chumba kimoja,” alisema mhudumu.
Mhudumu huyo alisema baada ya muda wa saa moja,
mvulana na mzee huyo wakaaga kwamba wanatoka huku wakisema kwamba msichana
amebaki chumbani akiwa amepumzika. Akithibitisha habari hizi, Kamanda Massawe
alisema taarifa ya tukio hilo ilitolewa na mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala
wageni katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni Jijini Tanga.
“Tatizo ni kwamba nyumba hii ya wageni wahudumu
wake hawakuwapa wageni hao daftari ili waorodheshe majina yao hivyo inakuwa
vigumu kuwafahamu,” alisema Kamanda Massawe na kufafanua kuwa alifariki
akitolewa mimba ya mwezi mmoja.
Kamanda Massawe alisema mpaka sasa hakuna mtu
aliyekamatwa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini
waliohusika na kifo hicho.
GAZETI LA
MWANANCHI Alhamisi Decemba 27, 2012
No comments:
Post a Comment