UMOJA WA WAKRISTO WATOA TAMKO ( Tanzania Daima 26/12/2012) |
.
JUKWAA la Wakristo nchini (TCF), limeeleza
kusikitishwa kwake na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya licha ya
kuwepo uchokozi na kashfa dhidi ya Ukristo vinavyodaiwa kuenezwa na baadhi ya
waumini wa Kiislamu.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa hilo limedai kuwa
kanisa liko katika vita ya kiroho, hivyo ni vyema waumini wote wakakumbuka
kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu ndiye mlinzi wa watu na kanisa lake na
jibu litapatikana kwa njia ya sala, kufunga na maombi.
Kauli hiyo nzito ilitolewa jana kwenye ibada ya
kitaifa ya Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini mjini Moshi na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa kanisa na kiserikali.
Tamko hilo zito la TCF, linajumuisha taasisi kuu
za umoja wa makanisa nchini ambazo ni Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya jukwaa hilo,
Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Martin Shao, alisema kuwa tamko hilo
lina mambo makuu manane ikiwemo masuala ya kuendelea kuombea amani ya taifa
ambayo imetikiswa kwa kiwango kikubwa.
Alisema tamko lao lililotokana na kikao chao cha
Desemba 6 mwaka huu, linalenga kuitaka serikali kukemea baadhi ya waumini wa
dini ya Kiislamu ambao wamekuwa na tabia ya uchochezi, kwani wanaweza kuhatarisha
amani ya nchi na wao kama umoja wa Wakristo, hawatakubali hali hiyo iendelee.
Hujuma ya kuchomwa makanisa
Askofu Shayo alisema tukio la kuchomwa moto
makanisa ni uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa na waumini wake wakiwa
hawana habari na bila maandalizi yoyote, hivyo ni muhimu kuanzia sasa,
Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.
Alisema katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo
na kashfa na uchokozi wa makusudi unaofanywa na baadhi ya waumini wa Kiislamu
hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Sehemu ya tamko hilo zito na la kwanza kutolewa
na umoja huo wa makanisa, ilieleza kuwepo kwa mbinu chafu ambazo zimekuwa
zikifanywa na baadhi ya waumini wa imani ya Kiislamu kutumia baadhi ya vyombo
vya habari vya dini kukashifu Ukristo, pamoja na kukaa vikao mbalimbali
kutaka kuwaua wachungaji na maaskofu.
Alisema hali hiyo inaleta wasiwasi, hivyo umefika
wakati sasa wa viongozi wa dini na waumini kujilinda wenyewe kutokana na na
mbinu za kutaka kuwaua.
Askofu huyo alisema kitendo cha Serikali ya Rais
Kikwete kukaa kimya, inatoa taswira mbaya, kwamba serikali inakubaliana na
kashfa, hujuma za kuchoma makanisa na mali za kanisa.
Alisema tamko hilo linaelezea kusikitishwa na
mahusiano ya Wakristo na Waislamu kuzorota kutokana na kauli ambazo zimekuwa
zikitolewa na baadhi ya Waislamu ambao wamekuwa wakifanya makongamano,
machapisho mbalimbali, mihadhara kwa lengo la kuchafua Ukristo, huku serikali
ikifumbia macho.
Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo
Tamko hilo pia lilieleza kuwa kumekuwa na hoja
kwamba serikali inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo, jambo ambalo si kweli.
Askofu Shayo alisema maneno hayo ni ushahidi wa
uwepo wa ajenda za waumini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano
maovu kutetea dhana potofu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za
binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na serikali.
“Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi
na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo! Kwa watu walio
makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu
serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri
Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa
Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi
hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo!
“Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi
ngazi za juu serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna
Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine
mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi
kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala wa kisheria na sio
vinginevyo,” alisema Askofu Shayo.
Matumizi hasi ya vyombo vya habari vya kidini
Tamko hilo lilivishambulia vyombo vya habari vya
kidini kwamba vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislamu kuukashifu Ukristo
na kuwachochea Waislamu, wakiwataka wawaue maaskofu na wachungaji, iwe kwa
siri au hadharani.
Askofu Shayo alisema japo serikali imesikia
kashfa na uchochezi huo hatarishi, imeendelea kukaa kimya, na kuwaacha
wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti.
“Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya
umakini wa dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna
hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waumini na
viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa serikali na viongozi waliopo
madarakani, endapo waumini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo
na waumini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana
baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inasababisha
kujiuliza kama je, huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini
kujilinda yeye mwenyewe na waumini wake dhidi ya wenye imani kali?” alihoji.
Mapendekezo
Kutokana na hali hiyo, TCF ilipendekeza kuwa
tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa ili kujenga heshima/staha
na utu wa kila mmoja.
“Tunaitaka serikali yetu na vyombo vyake vya
usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati
ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha
wanajamii.
“Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea
pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na dola, ni udhaifu mkubwa wa uongozi na
uwajibikaji.
“Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa
ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa
au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia
kwa uharibifu uliofanywa,” lilisema tamko hilo.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuanzishwa kwa
baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini
yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda
na kuiongoza serikali kutofungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira
na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote
havipotoshwi.
“Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislamu,
Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya
waumini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa
upendo.
“Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada
zetu, sote tutambue, tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za
watu wengine wanazoziheshimu na kuzitukuza.
“Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia
kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini
husika wakisaidiana na Usalama wa Taifa. Stahamala (kustahimiliana) ni
fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na
maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana,” lilisema
tamko hilo.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycap Pengo, naye amepigilia msumari kwa
kuiasa serikali kutofumbia macho mihadhara ya dini inayokashifu dini zingine.
Kardinali Pengo ambaye amepata kunukuliwa mara
kadhaa akielezea kukerwa kwake na mihadhara hiyo, alisema endapo itaendelea
kuachiwa, taifa linaweza kujikuta kwenye vurugu za kidini.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya Sikukuu
ya Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Bonaventura, Parokia ya
Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
Alisema mihadhara inayokashifu dini nyingine
haikubaliki kwani kila mtu anaabudu kwa imani yake.
“Mihadhara ya dini imekuwa ikitumika katika
kukashifu dini nyingine huku serikali ikiangalia na kushindwa kuwachukulia
hatua watu wanaotumia mihadhara hiyo kukashifu wengine. Hali hii ikiendelea
kuwa hivyo, tunaweza kujikuta tuko mahali pabaya,” aliasa Kardinali Pengo.
Alisema hakuna mtu mwenye haki ya kukashifu dini
ya mtu mwingine na kama serikali lazima ikemee mihadhara ya kukashifiana
ambacho kiini chake hafahamu kilipoanzia.
Kardinali huyo alisema tofauti za kidini zilizopo
nchini zisiwe chanzo cha kuvunjika kwa amani.
“Leo tumeona watu wanatengeneza mihadhara ya
kukashifiana hatujui chanzo cha hiyo mihadhara na tumeona siku za hivi
karibuni watu wanachoma makanisa moto, hivyo ni wajibu wa serikali kulinda
amani ya watu na mali zao,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuchomwa kwa makanisa serikali haiwezi
kusema sio jukumu lao wakati ina wajibu wa kuhakikisha wanalinda amani.
Mbali na kuionya serikali kuacha kufumbia macho
mihadhara ya kashfa, Kardinali Pengo pia aliwataka Wakristo wa kanisa hilo
wasiwe watumwa wa mali, kwani watu wenye mali kiasi wanaishi kwa amani katika
roho zao kuliko watu wenye utajiri mkubwa.
|
No comments:
Post a Comment