WANAUME NENDENI KLINIKI MTAMBUA
AFYA ZA WAKE ZENU`
Na
Mwandishi wetu
17th
March 2013
Wanaume wameshauriwa kushiriki kliniki ili waweze
kutambua afya za wake zao wanapokuwa wajawazito badala ya kuwatelekeza.
Ushauri huo ulitolewa jana na Meya wa manispaa ya
Dodoma, Emanuel Mwiliko, wakati alipokua akifungua kambi ya kupima afya kwa
akina mama na watoto mjini hapa.
Mwiliko alisema kuwa kumekuwapo na tatizo kubwa kwa
wanaume wengi nchini kuwa wazito kwenda kliniki hali inayosababisha wasiweze
kujua afya za wake zao wanapokuwa na matatizo.
Alisema kuwa ifike wakati wanaume wabadilike kutoka
katika mtazamo walio nao hivi sasa na kuanza kushiriki kuwapeleka wake zao
kliniki ili waweze kuzitambua afya za wenzi wao.
“Sisi akina baba tumekuwa mstari wa nyuma katika
kushiriki kliniki hivyo natoa wito tujitokeze katika kushiriki kliniki sisi na
wake zetu hali ambayo itatusaidia kujua afya zao zinaendeleaje,” alisema
Mwiliko.
Aidha alitoa wito kwa jamii kuwa karibu na akina
mama wajawazito ili kuhahakisha kuwa wanajifungua salama.
“Tuhahakishe kuwa tunafuatilia afya za akinamama
wajawazito kabla na baada ya kujifunga ili kuweza kuwasaidia katika kuwalea
watoto wao katika afya iliyo njema,” alisema.
Naye meneja wa hospitali ya Agha khan mkoani hapa
ambao wameandaa kambi hiyo ya kupima afya bila malipo kwa wananchi, Kibe Abel,
alisema kuwa lengo ni kuwasogezea wananchi huduma karibu.
Abel alisema kuwa huduma hizo zinatolewa kupitia
mradi wa tuunganishe mikono katika kuboresha afya ya mama na mtoto (JHI) kwa
ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA).
“Huduma tunazo zitoa ni kupima watoto na akimama
wajawazito pamoja na kutoa elimu jinsi gani akina mama wanaweza kunyonyesha na
namna ya kuwalea watoto wao katika afya nzuri,” alisema Abel.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment